IMETOKA HABARI LEO:
MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni za IPP,
Dk Reginald Mengi amejibu tuhuma zinazosambazwa kwa lengo la kumchafua
katika jamii, zikimhusisha na ufisadi kwenye sekta za madini, gesi na
mafuta. Pamoja na majibu ya shutuma hizo, Dk Mengi amesisitiza kuendelea
na azma ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria waliohusika na uchafuzi
huo, ili sheria ifuate mkondo wake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari jana, Dk Mengi alisema hajapata kufanya udalali katika vitalu vya
madini kama tuhuma hizo zinavyodai.
Alisema shutuma kwamba anafanya udalali
katika vitalu vya madini na kuwa anajiandaa pia kufanya udalali katika
vitalu vya mafuta na gesi, alizipokea kupitia barua pepe aliyotumiwa
Septemba 7 na mtu aliyejitambulisha kama ‘CCM Tanzania’.
Alisema pamoja na..............
ujumbe huo uliokuwa na
kichwa cha habari kisemacho: ‘ubinafsi/ufisadi wa Mengi na chuki/fitna
kwenye maendeleo’ kutumwa kwake, pia ulitumwa kwenye vyombo vya habari,
waandishi wa habari, mitandao ya kijamii na watu wengine wakiwamo
wanasiasa.
Ujumbe huo pamoja na mambo mengine
ulidai kuwa kampuni za Dk Mengi zinashikilia vitalu 59 vya madini vyenye
ukubwa wa meta za mraba 3,752.37 ambavyo vimeshindwa kuendelezwa, huku
Watanzania wakikosa mapato na ajira na kwamba sasa anataka vitalu vya
gesi na mafuta ili afanye udalali pia.
Sehemu ya ujumbe huo ikizungumzia vitalu
hivyo ilisema: “Amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza. Watanzania
wanakosa mapato na ajira … sasa anataka vitalu vya gesi na mafuta. Je
huu ndio uzawa? Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali
wa vitalu vya rasilimali zetu. Waelezeni Watanzania ukweli huu."
Akijibu, Dk Mengi alisema:
“Nimeona ni vema nitumie haki yangu ya
kujibu, lakini kwa wale wanaohusika kusambaza taarifa hizo kuchafua jina
langu, wajue kujibu kwangu hakuondoi haki yangu ya kuchukua hatua za
kisheria.
“Kuingizwa kwa vitalu vya madini katika
hoja ya gesi. Huo ni upotoshwaji wenye lengo la kututoa kwenye hoja ya
msingi ya rasilimali yetu ya gesi. Sijawahi kufanya udalali kwenye
vitalu vya madini.”
Alisema taarifa hizo ni za uongo na
zimepotoshwa kutoka kikao cha Bodi ya Shirikisho la Sekta Binafsi
Tanzania (TPSF) kilichofanyika Agosti 28 na kufuatiwa na mkutano wa
waandishi wa habari kilichozungumzia rasilimali zilizopo nchini.
“Mambo mengi yalizungumzwa katika kikao
hicho ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa Watanzania. Kuhusu uwezeshaji
Watanzania, mambo muhimu matatu yalijadiliwa na kutolewa mapendekezo.
Mambo hayo ni ununuzi wa umma, ardhi na uvuvi na gesi asilia.
“Kwenye mkutano na waandishi wa habari,
mimi Mwenyekiti wa TPSF, niliwasilisha maoni kuhusu ununuzi wa umma,
Makamu Mwenyekiti, Salum Shamte, aliwasilisha kuhusu sekta ya ardhi na
uvuvi na Mkurugenzi Mtendaji, Godfrey Simbeye, aliwasilisha kuhusu gesi
asilia.”
Mengi alisema TPSF ilisisitiza umuhimu
wa ushirikishaji Watanzania katika uchumi wa gesi na kushauri kusitishwa
ugawaji vitalu vya gesi hadi sera ya gesi itakapokuwa tayari.
Alisema wakati Simbeye akiwasilisha
maoni yao, alisema TPSF itaomba kukutana na Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo ili kuwasilisha mawazo na mapendekezo ya
taasisi hiyo.
Alisema hata hivyo, siku chache baadaye
Profesa Muhongo alijibu kupitia vyombo vya habari, kwamba mpango wa
kugawa vitalu vya gesi na kuingia mikataba utaendelea huku akisema hana
mpango wa kukutana na TPSF… ni kupoteza muda.
“Jambo la pili ambalo lilitokea ni mimi
binafsi kushambuliwa kana kwamba maoni yaliyotolewa kuhusu gesi ni maoni
yangu binafsi na si ya TPSF. Kuhusu tuhuma kwamba si mzalendo na ni
mbinafsi, Mengi alijitetea:
“Ningependa kupuuza tuhuma hizo
Watanzania wanafahamu ukweli. Vile vile ningependa kupuuza tuhuma za
ubinafsi na kuwa sipendi maendeleo ya Watanzania wenzangu, kwa hili pia
wanafahamu ukweli.
Alisema hapingi kuwapo wawekezaji wageni
katika sekta ya gesi, lakini kuna mambo mawili anayapigania ambayo ni
Watanzania kunufaika na rasilimali yao ya gesi na kuwapo kwa sera ya
gesi inayotoa kipaumbele kwa Watanzania.
“Mimi napenda maendeleo ya nchi yangu;
kwa hiyo hata siku moja siwezi kupinga uwekezaji au ubia na wawekezaji.
Ninachosimamia ni manufaa kwa nchi yangu,” alisema Dk Mengi.
TOA MAONI YAKO HAPA:
No comments:
Post a Comment