CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimeendelea kuwavuta wasanii kujiunga na chama hicho, ambapo
sasa wasanii wanne wa muziki wa kizazi kipya, maarufu Bongofleva na
filamu, wanatarajiwa kutangazwa kuhamia chama hicho wiki hii. Wasanii
hao wanadaiwa tayari kukubali kuingia kwenye chama hicho na wanatarajiwa
kutangazwa rasmi hadharani katika mkutano wa hadhara utakaofanyika
jijini Dar es Salaam.
Kukubali kwao kuingia katika siasa,
kunatajwa kutokana na ushawishi mkubwa uliofanywa na wabunge vijana wa
chama hicho, pamoja na Diwani wa CCM kutoka kata moja ya Wilaya ya
Kinondoni, ili chama hicho kivune kura za vijana katika uchaguzi mkuu wa
2015.
Wabunge hao wa Chadema na majimbo yao
katika mabano ni Halima Mdee (Kawe); Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini);
John Mnyika (Ubungo) na Joseph Mbilinyi, jina la kisanii Sugu (Mbeya
Mjini).
Habari kutoka kwa watu wa karibu na
wasanii hao pamoja na ndani ya Chadema, zinawataja wasanii hao kuwa ni......
wanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jaydee na wa miondoko ya Hip hop,
Selemani Msindi ama Afande Sele.
Taarifa zinawataja wengine kuwa ni
mwanamuziki Fredy Maliki maarufu Mkoloni na mwigizaji wa filamu, Jacob
Steven kwa jina la kisanii JB.
Inadaiwa wasanii hao lengo la kuingia
katika siasa kupitia chama hicho, ni kuwania ubunge ambapo Jaydee
anatajwa kutaka kugombea wilayani Musoma; Afande Sele Morogoro Mjini;
Mkoloni Jimbo la Tanga na JB Jimbo la Mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo gazeti hili lilipowatafuta
kuzungumzia taarifa hizo wote walikana ingawa wapo waliokiri
kushawishiwa kuingia kwenye chama hicho na viongozi wa Chadema na
wananchi, ili wagombee ubunge.
Afande Sele alikana kujiunga na chama
hicho na kusema hana taarifa hizo isipokuwa ni kweli ameshawahi kufuatwa
na viongozi wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, wakimtaka ajiunge na chama
hicho na agombee ubunge Morogoro Mjini.
“Nimeshafuatwa na viongozi wa Chadema wa
mkoa na kata nijiunge na chama hicho na nigombee ubunge …tena hata
vijana wengi na baadhi ya wazee wamenitaka nigombee ubunge kwa kupitia
Chadema lakini nimekataa.
“Pia Sugu ni mshikaji wangu na anapokuja
Morogoro, vijiwe vyake ndio vyangu naye vijana wameshamfuata
wakimwambia anishawishi nigombee ubunge kupitia Chadema, amekuwa
akiniambia vijana wananitaka lakini mimi sitaki, sijawahi kujiunga na
chama chochote na naona mbunge wa sasa (Abdulaziz Aboud) anafanya kazi
nzuri.
“Mimi sio mwanasiasa, lakini ni
mwanaharakati kupitia muziki na mtandaoni na nimekuwa nikitoa maoni
mengi na kukosoa lakini narudia si mwanasiasa na sijawahi kujiunga na
chama chochote,” alisema Afande Sele.
Vilevile amekanusha kushawishiwa na
viongozi wa kitaifa wa Chadema au wabunge, ingawa amekiri kuna wabunge
wa chama hicho kuwa ni marafiki zake wakiwemo Mbilinyi na Zitto.
Kwa upande wa Jaydee alisema hafuati
itikadi ya chama chochote cha siasa na hapendi siasa kutokana na imani
kuwa siasa ni uongo na yeye hapendi uongo. Alisema hana nia ya kujiunga
na chama chochote cha siasa wala kugombea ubunge kupitia chama chochote.
Hata hivyo alipoulizwa iwapo atagombea baada ya Katiba kuruhusu mgombea binafsi, alisema kwa wakati huo atajua.
Hata hivyo, Licha ya kuwaona wanasiasa
ni waongo, anakiri wapo wanasiasa anawaamini kutokana na kazi zao na
kumtaja miongoni mwao ni Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Mbunge wa
Afrika Mashariki, Shy-rose Bhanji.
Mwanamuziki huyo alisema licha ya kuwa
na marafiki wa Chadema na CCM kama Sugu na Profesa Jay wa Chadema na
Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na Bhanji wa CCM, hawajawahi
kumshawishi kujiunga na vyama vyao.
Mkoloni Akizungumzia taarifa hizo za
kujiunga na Chadema, JB alikana na kusema; “mimi na siasa ni vitu
tofauti, sijawahi kufuatwa na mtu wa Chadema na angalau kungekuwa na
dalili basi uniulize, hiyo ni taarifa ya kutengenezwa na wewe ndiye
uliyetengeneza hakuna aliyekupa ni udaku huo.”
Kwa upande wa Mkoloni, alisema hajawahi
kufuatwa wala kushawishiwa kujiunga na chama chochote, isipokuwa ni
mwanachama wa muda mrefu wa Chadema na amekuwa akishiriki kampeni,
mikutano ya hadhara na matukio yote ya uhamasishaji ndani ya chama
hicho. Alisema kuhusu kuombwa kuwania jimbo mkoani Tanga kwa tiketi ya
chama hicho, alisema hajawahi kuombwa na chama hicho kufanya hivyo.
“Sijawahi kuombwa nigombee jimbo, na
kuhusu nia ya kugombea, ni mapema mno kuzungumzia suala hilo sasa na
hata kanuni za chama changu haziruhusu labda uniulize swali hilo mwakani
naweza kuwa na jibu,” alisema Mkoloni.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa, alikataa kuzungumzia taarifa hizo akidai yuko
barabarani na masuala yote yanayohusu chama hicho aulizwe Msemaji wa
chama hicho.
Hata hivyo msemaji wa chama hicho,
Tumaini Makene alisema hana taarifa kuhusu kufanyika kwa mkutano wa
chama hicho Dar es Salaam na kutaka apewe muda afuatilie taarifa hizo.
TOA MAONI YAKO HAPA:
No comments:
Post a Comment