MWENYEKITI wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema Watanzania wengi wanazidi kuwa masikini kwa sababu hawazitumii fursa za utajiri uliopo nchini, hivyo kutaka vijana kuona kwa macho fursa hizo ili waweze kujikwamua kutoka kwenye dimbwi hilo la umasikini.
Akizungumza wakati wa kutoa zawadi kwa washindi watatu wa shindano la nini kifanyike kuzalisha ajira nyingi hapa nchini aliloanzisha Mwenyekiti huyo wa IPP, Mengi alisema baada ya Watanzania kupofushwa kuwa nchi yao ni masikini, wengi walibweteka na kushindwa kuchangamkia fursa zilizopo hali ambayo imeifikisha nchi hapa ilipo.
Alisema jambo la msingi kwa vijana wa Tanzania ni kuibua mawazo ya shughuli gani atafanya badala ya kukimbilia namna ya kupata mitaji, kwani wengi ambao wamekimbilia kutafuta mitaji wamejikuta wanaipata mitaji hiyo, lakini wakashindwa namna ya kuitumia.
Washindi katika shindano hilo ambalo limeanzishwa na Mengi lijulikanalo kama Tweet Bora ni Lilian Wilson wa Chuo Kikuu cha Ardhi aliyepata Sh milioni moja, Susan Senga ambaye ni mfanyabiashara ndogo alipata Sh 500,000 na Ombeni Kaaya ambaye ni mjasiriamali kutoka Nzega, Tabora aliyekabidhiwa Sh 300,000.
Katika maoni yao, Lilian alipendekeza kuwa ili kuondoa tatizo la ajira wajasiriamali waliofanikiwa na Serikali waanzishe mifuko ya kuwekeza mitaji kwenye biashara za vijana zenye uwezekano wa kukua haraka badala ya kutegemea mikopo ya benki au taasisi za fedha.
Susan Senga yeye alipendekeza kuanzishwe vipindi maalumu kutoa elimu ya ujasiriamali ya kuwawezesha vijana kuwatoa katika fikra ya kuishi kutegemea ajira ili kujiairi.
Kwa upande wake, Ombeni Kaaya katika maoni yake alisema tafiti wanazofanya wanafunzi wa elimu ya juu mwaka wa mwisho zihusu jinsi watakavyojiajiri katika fani zao kwani itasaidia wengi wajiajiri.
Naye Dk Donath Olomi wa Taasisi ya Management and Entrepreneurship Development ambao ndio wanaoteua washindi, alisema katika shindano la mwezi huu jumla ya maoni 979 yalipokewa na watachagua washindi watatu kutoka katika maoni hayo.
TOA MAONI YAKO HAPA:
No comments:
Post a Comment