BAADA ya bendi mama ya wanamuziki wengi
ya Twanga Pepeta, kumrudisha kundini mwanamuziki aliyekuwa akifanya
vizuri katika bendi ya mapacha watatu, Kalala Junior, imeamua kufanya
harakati zake za mikoa ya Iringa
na Mbeya.
Siku ya kwanza Twanga Pepeta inataraji kufanya onyesho
mkoani Iringa tarehe 14-09-2012 siku ya Ijumaa katika ukumbi wa Highland.
Kesho yake siku ya Jumamosi tarehe 15-09-2012
watakuwa Jijini Mbeya ndani ya City Pub na siku ya Jumapili tarehe 16-09-2012
watamalizia kufanya ziara ya maonyesho katika ukumbi huo huo wa City Pub
kwa kufanya Bonanza maalum kwa ajili ya wakazi wa Jiji la Mbeya na maeneo ya
jirani.
Matayarisho yote muhimu ya ziara hii ya maonyesho
yamekamilika na Bendi inataraji kuondoka mara baada ya kumalizika kwa onyesho
la kila siku ya Alhamisi tarehe 13-09-2012 linalofanyika Club Maisha Oysterbay.
Bendi inataraji kurudi mara tu baada ya onyesho la
mwisho litakalofanyika siku Jumapili tarehe 16-09-2012 Jijini Mbeya.
Twanga Pepeta itakapokuwa katika ziara, Itamtambulisha
Mwimbaji wao mpya Kalala Jr aliyerejea hivi karibuni kutoka katika Bendi
ya Mapacha Watatu.
Sambamba na utambulisho huo pia itatambulisha nyimbo
zao mpya za “Ngumu Kumeza” ilyotungwa na Mirinda Nyeusi, “Nyumbani ni
Nyumbani” iliyotungwa na Kalala Jr, “Walimwengu” iliyotungwa na Jumanne Said
na ” Mapambano ya Kipato” iliyotungwa na Mwinjuma Muumini.
Mara baada ya kurejea Twanga Pepeta itaendelea kufanya
maonyesho yake kama kawaida Jijini Dar es salaam katika kumbi za Club
Billicanas siku ya Jumatano, New Club Maisha siku ya Alhamisi, Free Time Resort
Ukonga Banana, Mango Garden siku ya jumamosi na Jumapili mchana Leaders Club na
usiku Mzalendo Pub.
MUDDY K
EVENTS MANAGER
No comments:
Post a Comment